21 Juni 2023 - 17:14
Kudhalilishwa jeshi la Israel huko Jenin, ukurasa mpya katika kitabu cha mapambano ya Palestina

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel majuzi walilazimika kutumia jeshi la anga kushambulia kwa mabomu wanaharakati wa Kipalestina katika mji wa Jenin ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Israel ilichukua hatua hiyo baada ya kukabiliana na mapambano makali ya wapigania uhuru wa Palestina ambapo vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimelazimika kukiri kwamba mapambano ya wanaharakati wa Palestina Jumatatu iliyopita kwenye mji wa Jenin yalikuwa tata na ya kipekee.

Saraya al-Quds, tawi la kijeshi la harakati ya Jihad Islami ya Palestina imetangaza kuwa, vikosi vya muqawama vilifanikiwa kulipua gari la kijeshi la Kizayuni na kuliangamiza. Wazayuni walikiri kwamba, askari wa utawala huo walinaswa katika shambulizi la kuvizia la wanamapambano wa Palestina na saba kati yao walijeruhiwa. Kwa sababu hiyo, helikopta za utawala wa Kizayuni zilitumwa kwenye eneo la mapigano hayo kuokoa maghasibu hao.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza baada ya miaka 20 ya Intifadha ya Pili ambapo jeshi la Israel lilitumia jeshi la anga kuushambulia kwa mabomu mji wa Jenin ulioko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Matumizi ya jeshi la anga kushambulia mji wa Jenin yalitokea baada ya kudhihiri waziwazi udhaifu wa jeshi la Israel dhidi ya muqawama wa wanamapambano wa Palestina. Kanali ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni imeripoti kuwa: Shambulio la anga dhidi ya Jenin lilitekelezwa kwa ombi la wanajeshi waliokuwa katika uwanja wa vita na kuzidiwa wa wapigania uhuru wa Palestina. Kwa hakika jeshi la Israel lililazimika kutumia kikosi cha anga ili kuokoa askari waliokuwa wamezingirwa na Wapalestina.

342/